
Vipele hivyo hutokea wakati vishimo vya kupitisha jasho katika ngozi vinapozibwa kwa mafuta au seli za ngozi zilizokufa au wadudu, yaani bakteria.
Kwa lugha ya kidaktari, chunusi inaitwa ‘Acne Vulgaris.’ Ni ugonjwa wa ngozi unaomuathiri binadamu kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano, nchini Marekani pekee, inaelezwa kuathiri watu zaidi ya milioni 17.
Chunusi inaweza kujitokeza katika umri wowote wa binadamu, lakini ina kawaida ya kuwaathiri sana vijana, hasa katika umri wa balehe (adolescence)
Barafu
Hii ni dawa inayoweza kupunguza chunusi zionekane ndogo na kupunguza madhara yanayosababishwa.
Namna ya kutumia barafu kutibu chunusi ni rahisi na haraka zaidi. Chukua kipande cha barafu na ukipitishe sehemu zilipo na chunusi mara kadhaa kwa wastani wa dakika tatu hadi tano.
Pia, mwenye chunusi ukumbuke kusafisha vizuri uso wako, kabla ya kuanza kupitisha hiyo barafu kwenye uso wako.
Kitunguu swaumu
Hii inajulikana kama kitu cha kushangaza katika tiba. Huko Mashariki ya mbali, inafananishwa na miujiza. Hiyo ni kwa sababu ina nguvu za kuua bakteria mbalimbali na kuzuia magonjwa, ikiwemo kutibu chunusi.
Kuna namna mbili ya kutumia kitunguu swaumu katika tiba ya chunusi. Namna ya kwanza ni kukitumia kitunguu swaumu kwenye vyakula vinavyopikwa kila siku na namna ya pili, ni kukitwangwa kitunguu swaumu na kukipaka moja kwa moja katika sehemu yenye chunusi.
Mbali na harufu yake isiyopendwa na wengi, kitunguu swaumu, kina uwezo wa kumpa mtu afya na urembo unaouhitaji. Kinasaidia kupunguza ukubwa wa chunusi.
Hata hivyo, unahitajika umakini, kwani kitunguu swaumu kinaweza kuunguza ngozi yako, usipokuwa makini na ili kuepuka, jaribu kuchanganya kidogo na maji baada ya kukitwanga, ili kupunguza makali yake.
Limao
Dawa nyingine nzuri kwa ajili ya chunusi usoni na mwilini ni limao. Hiyo inapatikana kwenye vyakula vingi, mathalan haikosekani kwenye lishe ya supu au mapishi kama ya samaki.
Limao lina kiasi kingi cha vitamini C, inayoweza kutumika kama antibaiotiki inayozuia kuongezeka na kuua bakteria wanaosababisha chunusi. Pia, ina tindikali maalumu inayohamasisha chunusi kutoka katika ngozi.
Kinachotakiwa kufanywa ni kwamba, mtu anakata limao katika pande mbili au nne na kisha anapaka maji yake taratibu kwenye chunusi kwa wastani wa dakika 10, kisha anajisafisha na maji safi. Tindikali katika limao linaweza kuzidhuru seli zilizopo juu ya ngozi yako, hivyo tumia dawa hiyo mara moja au mbili kwa wiki na siyo kila siku.
Vitamini C iliyomo kwenye limao husaidia kukinga mwili dhidi ya magonjwa mengi, sababu ndiyo vitamini inayosaidia kuongeza kinga ya mwili. Kinga ni bora. Hivyo, inaaswa kutumia lishe ya vitamini C kila mara au kunywa juisi ya limao kila siku, ili kuuweka mwili katika afya bora zaidi muda wote.
Mshubiri (Alovera)
Mshubiri au Alovera kama ilivyozoeleka na namna nzuri kwa wote wanaotaka kubaki na ngozi nyororo na ya kupendeza kila siku.
Unafanyaje? Chukua kipande cha mshubiri ‘freshi’ na ukikate, kisha chukua maji yake na kupaka moja kwa moja usoni huku ukijisugua polepole kwa muda wa kati ya dakika 15 hadi 20, kisha kujisafisha na maji safi.
Dawa hiyo inatumiwa mara mbili hadi tatu kwa wiki. Hiyo ndiyo njia rahisi ya kutibu chunusi bila kukuacha na madhara mengine mabaya.
Dawa ya meno
Dawa ya meno ni nyenzo nyingine ya asili mtu anaweza kutumia kujitibu chunusi. Hii inatumika usiku tu. Paka kiasi kidogo cha dawa hiyo kwenye chunusi kisha lala nayo, inapofika asubuhi jisafishe na maji safi. Hilo linaloaswa kufanyika kila baada ya siku moja, hadi mgonjwa wa chunusi anapopona.
Tango
Hilo ni tunda, mboga pia chanzo kizuri cha kiini cha potasiamu na vitamini nyingi ambazo zina kazi muhimu katika ngozi ya binadamu. Ina kawaida ya kuifanya ngozi ionekane laini na inayopendeza.
Tango ni mojawapo ya dawa kamili za kutibu chunusi na rahisi katika kulitibu chunusi. Unaanza kwa kulikata tango katika vipande vidogo mfano wa slesi na kisha inabandikwa juu ya ngozi yenye chunusi.
Kumbuka kwanza kusafisha kwanza Ngozi yako, kabla ya kubandika hizo slesi za tango. Namna nyingine ni ya kusaga tango, upate juisi yake na uchanganye na sukari kisha ujisuguwe nazo kwenye ngozi yenye chunusi kwa dakika walau mbili hadi tatu na unamalizia kwa kujisafisha na maji safi.
Asali
Asali mbichi ya asili ni dawa nzuri sana ya kutibu chunusi. Ina antibaiotiki ya asili inayosaidia kupunguza ukubwa wa chunusi na maumivu yake.
Pia, asali inaweza kuzuia ngozi isipatwe na maambukizi mengine, ambayo yangeweza kusababisha matatizo kwenye ngozi au makovu. Hivyo, asali inachukuliwa kama sehemu ya dawa za asili nzuri zinazotibu chunusi.
Inavyotumiwa, anza kwa kusafisha ngozi vizuri na maji ya vuguvugu na kisha jipake asali moja kwa moja kwenye sehemu yenye chunusi. Acha kwa dakika 30 na kisha jisafishe na maji safi ya vuguvugu.
Dawa hiyo inatumika ama mara mbili au tatu, ndiyo inakuwa katika nafasi nzuri ya kutoa majibu sahihi ya kitabibu.
Mvuke
Huo unasaidia kusafisha ngozi. Ni rahisi sana kutumia mvuke kutibu chunusi.
Mchakato wake unaaza kwa kuchemsha maji kwenye chombo kilichofunikwa na inaachwa sufuria nafasi kidogo ya mvuke kutoka. Mtu anachofanya anachukua taulo kidogo na kisha anajifunika usoni, huku akisogelea karibu na mvuke unapokea na kuruhusu umpate kwa mbali.
Baki hapo kwa dakika tano hadi 10, huku ukiwa umetulia ‘relax.’ Huu mvuke utakusaidia pia kujisikia mtulivu na kukuondolea mfadhaiko wa akili. Unapomaliza hakikisha unajisafisha kwa maji safi yaliyo baridi.
Papai
Dawa nyingine madhubuti ya chunusi ni papai. Tunda hilo ni moja ya matunda yanayotumika kwa ajili ya urembo kwa kinamama.
Hatua zake ni papai linachukuliwa na inachanganywa na asali kidogo, linakorogwa kidogo na kisha kujipaka sehemu yenye chunusi kusugua kwa dakika 15. Baada ya hapo, unatakiwa kujiosha usoni na maji ya moto na baada ya kumalizia, rudia kujisafisha kwa maji baridi. Hilo linatakiwa kufanyika kwa wastani wa mara mbili mpaka tatu kwa wiki.
Ute mweupe wa yai
Hiyo inaweza kuchukuliwa kama njia rahisi na isiyo na gharma katika kutibu chunusi. Kwa mujibu wa wanasayansi, kutumia mchanganyiko wa ute mweupe wa yai na maji ya limau, ni namna nzuri ya kutibu chunusi.
Changanya ute mweupe wa mayai matatu na kijiko kidogo kimoja cha maji ya limau na ukoroge vizuri. Pakaa mchanganyiko huo usoni na uache kwa dakika 15, kisha jisafishe na maji ya moto.
Hilo nalo linaloshauriwa kufanywa kati ya mara moja au mbili kwa wiki.